Kamati Kuu ya Chama cha ODM imemuidhinisha Seneta wa Siaya Dkt. Oburu Oginga kuwa kinara mpya wa chama cha ODM.
Dkt. Oginga anajaza pengo lililoachwa na aliyekuwa kinara wa ODM Raila Odinga aliyefariki Oktoba 15 wakati akipokea matibabu nchini India.
Nalo azimio hilo limeafikiwa wakati mkutano wa kamati hiyo uliofanywa leo Jumatatu.
Huo ni mkutano wa kwanza wa kamati hiyo kuwahi kufanyika tangu kifo cha Raila ambaye pia aliwahi kuhudumu kama Waziri Mkuu wa nchi.
Kamati ikitumia fursa hiyo kuomboleza kifo cha kigogo huyo wa siasa za Kenya.
“Kwamba tunaelezea shukrani zetu za dhati kwa watu na serikali ya Kenya kwa msaada, upendo na umoja mwingi uliotolewa kwa kiongozi wetu na familia yake kufuatia kifo chake,” ilisema taarifa ya kamati hiyo iliyotiwa saini na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna.
“Kwamba tunamuidhinisha Dkt. Oburu Oginga kuwa kiongozi mpya wa chama na kutoa wito kwa wanachama wote kumuunga mkono na kushirikiana naye ili kumwezesha kuongoza chama wakati huu mgumu,” iliongeza taarifa hiyo ambayo pia ilituma risala za rambirambi kwa familia ya Raila, marafiki zake ndani na nje ya Kenya na kwa Wakenya wote kwa jumla kufuatia kifo cha Raila.
Taarifa hiyo ikiashiria kuwa mkutano wa kuadhimisha miaka 20 tangu kuasisiwa kwa ODM utaendelea kama ilivyopangwa.
Mkutano huo wa siku tatu utafanyika kati ya Novemba 14-16 katika kaunti ya Mombasa.
Awali, mkutano huo ulipangwa kuongozwa na Raila ambaye aliugua na kulazimisha kuaihirishwa kwake.
Kifo chake kikimaanisha kwamba Raila hatapata fursa ya kuongoza mkutano wa kusherehekea miaka 20 tangu kuanzishwa kwa chama cha ODM alichokipigania kwa udi na uvumba.
