Paul Biya atangazwa mshindi wa uchaguzi Cameroon

BBC
By
BBC
2 Min Read
Rais Paul Biya atangazwa mshindi wa Urais nchini Cameroon

Baraza la katiba la Cameroon limemtangaza Rais aliye madarakani Paul Biya kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais kwa karibu asilimia 54% ya kura.

Kwa mujibu wa matokeo rasmi, Biya alipata asilimia 53.66 ya kura, huku mpinzani wake mkuu na aliyekuwa mshirika wake wa zamani, Issa Tchiroma Bakary, akipata asilimia 35.19.

“Mgombea Biya Paul ametangazwa kuwa Rais wa Jamhuri, baada ya kupata wingi wa kura halali zilizopigwa,” alisema Clement Atangana, Rais wa Baraza la Kikatiba.

Ushiriki wa wapiga kura ulikuwa asilimia 57.76, huku asilimia 42.24 wakijiondoa katika mchakato wa kupiga kura.

Jumla ya watu zaidi ya milioni nne walishiriki katika uchaguzi huo. Wagombea kumi walikuwa wakigombea urais, na Biya ambaye hajawahi kushindwa katika uchaguzi wowote tangu aanze kutawala mwaka 1982 alionekana tangu awali kuwa na nafasi kubwa ya kushinda.

Hata hivyo, matokeo haya yanapingana na madai ya Issa Tchiroma, ambaye kabla ya matokeo rasmi kutangazwa, alijitangaza kuwa mshindi wa uchaguzi huo.

Katika mahojiano ya hivi karibuni na BBC, Tchiroma alisisitiza kwamba amemshinda bosi wake wa zamani, Paul Biya, akidai kwamba uchaguzi ulighubikwa na udanganyifu mkubwa na dosari za wazi katika uendeshaji wake.

Madai hayo yamechochea hasira na maandamano katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo hadi sasa watu wasiopungua watano wameripotiwa kuuawa.

Waandamanaji wengi wamekuwa wakisisitiza madai ya Tchiroma kwamba yeye ndiye mshindi halali.

Serikali imetaja maandamano hayo kuwa haramu, na imewakamata viongozi kadhaa wa upinzani pamoja na wanaharakati.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaonya kuwa wimbi hili jipya la maandamano linaweza kuisukuma Cameroon, taifa lililokuwa likijulikana kwa utulivu wake wa kisiasa, kuelekea kwenye ghasia na machafuko ya kisiasa endapo matokeo ya uchaguzi hayatakubalika kama yanayoakisi matakwa ya wananchi.

Biya aliingia madarakani kwa mara ya kwanza mnamo 1982, matokeo haya ya uchaguzi sasa yanamaanisha kuwa ataendelea kutawala hadi 2032.

BBC
+ posts
Share This Article