Mwanamuziki wa Tanzania Barnaba Classic ametangaza kwa msisimko, mpango wa kuzindua studio yake iliyokarabatiwa, Ijumaa usiku kuamkia Jumamosi hii.
Hii ni baada ya studio hiyo ambayo pia ni afisi yake kuungua yapata siku 35 zilizopita.
Alichapisha video inayoonyesha tukio hilo la ajali ya moto ambapo wahudumu wa zima moto wanaonekana kujizatiti kujaribu kuuzima moto huo naye Clasic akitizama kwa huzuni.
“Maisha yana changamoto nyingi, na kama mwanadamu lazima uzipitie. Lakini badala ya kulalamika, simama, jinyanyue na songa mbele. Tafuta suluhisho, rekebisha kinachokuzuia, kisha endelea” alishauri msanii huyo kwenye ujumbe wake.
Alitoa shukurani kwa Mungu kwa kila hatua na kila changamoto aliyopitia akisema zote zimemjenga kuwa imara zaidi na kumfanya aendelee kupambana.
“Leo zimetimia siku 35 bila screen, bila muziki, bila kurekodi, bila kurudi kwenye mazoea yangu ya kawaida… lakini ndani yake nimejifunza zaidi kuliko nilivyowahi kufikiria,” alisema Classic.
Msanii huyo wa muda mrefu alidhihirisha furaha kubwa alipotangaza uzunduzi huo wa usiku wa manane Ijumaa akielezea kwamba Jumamosi itakuwa siku yake ya kuzaliwa pia akiahidi kuletea mashabiki zake mwonekano mpya wa studio hizo.