Tamasha maarufu nchini Uganda ambalo liliahirishwa mwezi februari mwaka huu la Roast and Rhyme litaandaliwa Juni Mosi, 2025.
Hafla hiyo ya kila mwaka huhusisha muziki, chakula cha Uganda pamoja na mitindo ya kitamaduni.
Awamu ya mwaka huu inayohusu muziki aina ya Reggae na Ragga itaandaliwa katika eneo la Lugogo jijini Kampala tofauti na wamu za wali.
Julius Kyazze, mmoja wa waandalizi wakuu wa tamasha hilo ambaye pia ni mmiliki wa kampuni ya muziki ya Swangz Avenue alielezea kwamba walihamishia tamasha hilo eneo ambalo litakuwa rahisi kwa wengi kufika.
Mabadiliko hayo yanatoa matumaini ya mambo mazuri katika tamasha hilo ambapo watakaohudhuria watakuwa na eneo la kutosha la maegesho ya magari na usalama wa hali ya juu.
Kwa mara ya kwanza kabisa waandalizi wametenga eneo la watu mashuhuri zaidi ambalo tiketi zake zitakuwa ghali kuliko maeneo mengine.
Eneo hilo litakuwa la starehe zaidi na litakuwa pia naviwambo vya kipekee huku tiketi moja ya eneo hilo ikiuzwa kwa shilingi elfu 150 za Uganda sawa na shilingi elfu 5300 za Kenya.
Wanamuziki ambao wamepangiwa kutumbuiza siku hiyo ni pamoja na Winnie Nwagi, Karole Kasita, Beenie Gunter na wengine wengi.
Hatua hii ni afueni kwa wale ambao walinunua tiketi za tamasha ambalo halikufanyika mwezi Februari kwani tiketi zao zinaweza kutumika Juni Mosi.