Jaydee azindua wimbo mpya

Wimbo huo kwa jina Popo unaangazia safari yake katika muziki huku akitoa shukrani.

Marion Bosire
2 Min Read
Lady Jaydee

Mwanamuziki wa muda mrefu wa Tanzania Judith Wambura Mbibo maarufu kama Lady Jaydee amezindua wimbo mpya kwa jina Popo.

Wimbo huo wa mtindo wa Reggea ambao ndio wake wa kwanza mwaka huu wa mwaka 2025 unaangazia safari yake katika tasnia ya muziki anapojiandaa kusherehekea miaka 25 katika muziki almaarufu ‘Silver Jubilee’.

Katika kuadhimisha miaka 25 katika muziki, Jaydee ameahidi pia kushirikiana na wanamuziki mbali mbali hasa katika kurudia nyimbo zake za wali au ukipenda remix.

“Remix ya kwanza naitoa Ijumaa ijayo. Kuna wasanii watatu tofauti wa Hip Hop nimefanya nao. Kila wiki natoa ya msanii tofauti.” aliandika Jaydee kwenye Instagram huku akiwapa wafuasi wake changamoto.

Aliwahimiza wabashiri wasanii ambao ameshirikisha kwenye remix zake na atakepata atazawadiwa tiketi moja ya kuhudhuria tamasha lake la Silver Concert na atakubaliwa pia kuhudhuria siku ya mapishi.

Jaydee ameandaa hafla kadhaa za kusherehekea miaka 25 katika muziki ya kwanza ikiwa tamasha la Silver Concert litakaloandaliwa Juni 13, 2025 katika eneo la Super Dome jijini Dar es Salaam.

Ataandaa hafla nyingine ya kusherehekea miaka 25 ya muziki pamoja na nyingine ya mapishi.

Lady Jaydee ambaye ana umri wa miaka 45 sasa alitoa albamu yake ya kwanza kwa jina ‘Machozi’ mwaka 2000 wakati akianza kazi rasmi kama mwanamuziki.

Albamu zake nyingine ni pamoja na Binti ya mwaka 2003, Moto ya mwaka 2005, Shukrani ya mwaka 2007, The Best of Lady Jaydee ya mwaka 2012, Nothing But The Truth ya mwaka 2013, Woman ya mwaka 2017 na 20 aliyotoa mwaka 2021 kuadhimisha miaka 20 katika muziki.

Website |  + posts
Share This Article