Mwanamuziki wa Nigeria Waje alihojiwa kwenye kipindi cha mitandaoni kiitwacho “The Honest Bunch” ambapo alifichua kwamba sauti ya kike inayosikika kwenye wimbo wa P Square ‘Do Me’ ni yake.
Katika mahojiano hayo, mwimbaji huyo alifichua pia kwamba hakuwahi kulipwa chochote na kundi hilo la muziki la kaka wawili na hakuwahi pia kutambuliwa kwa kuimba nao wimbo huo wa mwaka 2007.
Waje alisema wakati wa wimbo huo kutolewa yeye alikuwa chipukizi na hakuwa amepata ufahamu kuhusu mambo yanavyofanywa katika tasnia ya muziki na aliimba sehemu ya wimbo huo bila mapatano ya aina yoyote.
Msanii huyo aliwachekesha waliokuwa wakimhoji kwamba hakuna aliyemwamini kwamba ni yeye mwimbaji wa pambio ya wimbo huo kwani hakuwa amepata umaarufu.
Alikumbuka wakati mmoja akiwa sokoni huko Onitsha ambapo alisikia wimbo huo ukichezwa na alipoambia watu kwamba ni yeye ameimba hawakuamini wakidhania alijitakia tu makuu.
Kibao cha “Do Me” ni kati ya vile maarufu zaidi vya kundi la P Square ambalo kwa sasa limevunjiliwa mbali.
Waje ambaye jina lake halisi ni Aituaje Aina Vivian Ebele Iruobe, aliinuka na kuwa mmoja wa wasanii wa kike bora zaidi nchini Nigeria.
Ana albamu nne ambazo ni W.A.J.E ya mwaka 2013, Red Velvet ya mwaka 2018, Heart Season ya mwaka 2021 na WAJE 2.0 aliyotoa mwaka 2022. Amewahi kuteuliwa kuwania tuzo mbali mbali ndani na nje ya Nigeria
