Mawakili wa mwanamitandao maarufu na mfanyabiashara wa Tanzania Jenifer Bilikwiza Jovin maarufu kama Niffer wameelezea kwamba yuko salama kizuizini.
Katika taarifa rasmi, mawakili hao wakiongozwa na Peter Kibatala walielezea kwamba Niffer yuko salama katika seli za polisi licha ya hali ilivyokuwa nchini Tanzania katika muda wa siku chache zilizopita.
Walisema kwamba hali ambayo imekuwepo imewazuia kutekeleza majukumu yao kwa mteja huyo huku wakiomba wafuasi wake wawe na subira.
“Tutakuja na mrejesho wa kisheria kwa wakati mwafaka” alisema Wakili Kibatala.
Haya yanajiri siku kadhaa baada ya maafisa wa polisi jijini Dar es Salaam nchini Tanzania kuelezea sababu za kumkamata Niffer, ambaye wengi walidhani alitekwa nyara.
Kamanda wa Polisi katika kanda maalum ya Dar es salaam Jumanne Muliro wakati huo alielezea kwamba makosa yanayomkabili Niffer ambaye ana ushawishi mkubwa mitandaoni ni pamoja na kuhamasisha wananchi kufanya fujo siku ya uchaguzi.
Makosa mengine aliyotaja Muliro ni kuhamasisha watu kuchoma vituo vya kuuza mafuta, kuhimiza watu kushambulia maafisa wa polisi na vitendo vingine vya vurugu.
Niffer anaaminika kuendesha uhamasisho huo mitandaoni na kupitia njia nyingine ambazo Muliro alisema zitathibitishwa mahakamani.
Niffer alikamatwa kutoka eneo lake la biashara huko Sinza.
