Tume ya Uwiano na Utangamano wa Taifa, NCIC, imekanusha madai ya kuvunjwa kwake.
Mwenyekiti wa tume hiyo Rev. Dkt. Samuel Kobia ametaja taarifa za kuvunjwa kwa tume hiyo hususan zilizoenezwa na chombo kimoja cha habari nchini kuwa za kupotosha.
“Kwa hivyo, tunataka kubainisha kuwa ripoti za vyombo vya habari hasa Nation zikidai tume hii imevunjwa siyo sahihi, ni za kupotosha, na uwasilishaji visivyo wa ukweli,” alisema Dkt. Kobia kwenye taarifa.
“Tume bado ingalipo na inaendelea kutekeleza majukumu yake ya kisheria.”
Dkt. Kobia akiongeza kuwa kwa sasa wanatayarisha ripoti itakayokabidhiwa Rais William Ruto baada ya muhula wa makamishna wa sasa kumalizika Novemba 17 mwaka huu.
Makamishna hao waliteuliwa miaka 6 iliyopita.
Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen tayari ameteua jopo la kuongoza mchakato wa kuteua makamishna wapya.
