Rais William Ruto amesisitiza umuhimu wa kujenga uwanja mpya wa kisasa wa ndege nchini akilalamikia kuchakaa kwa Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta, JIKA.
Juhudi za kujenga uwanja mpya kupitia ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi awali zilikumbana na pingamizi kali huku makubalino yaliyokuwa yamefikiwa na kampuni ya Adani iliyotarajiwa kustawisha uwanja huo yakifutwa.
“We need to build a new airport. Tuwache upuuzi! We need to build a new airport. Friends, honestly. Sasa kitu yetu iko pale JKIA, canvass iko kwa runaway, sasa tunaongea nini?” aliuliza Rais Ruto akiwa jijini Doha, Qatar wakati akiwahutubia Wakenya wanaoishi nchini humo pembezoni mwa Mkutano wa Maendeleo ya Jamii wa Umoja wa Mataifa.
“Qatar hapa inajenga uwanja wa ndege nchini Rwanda chini ya mpangokazi sawia. Tuko pamoja? Kwa hivyo nilikuwa na mazungungumzo na Sheikh leo, na tumeweka mezani kile tunaenda kufanya na uwanja wetu wa ndege, tunaenda kufanya nini na Kenya Airways na masuala mengine yote kwa sababu aina ya uwekezaji ambao tunahitaji kwa huo uwanja wetu wa ndege yamkini ni takriban shilingi bilioni 200 za Kenya.”

Rais Ruto akitumia fursa hiyo kusema serikali inawawezesha Wakenya walio ughaibuni kuendelea na kuchangia kwa ukuaji wa taifa.
Aliongeza kuwa serikali imeimarisha huduma za ughaibuni, kupunguza muda wa utengenezaji wa pasipoti mpya kutoka miezi mitatu hadi siku tatu tu kwa wale ambao wana ofa za kazi, na inafanya matayarisho ya safari zao ili kuchukua fursa hizo.
Na ili kulinda wafanyakazi wa Kenya, kiongozi wa nchi alisema usajili wa mashirika laghai 600 yanayowasajili Wakenya wanaotaka kufanya kazi ughaibuni umefutuliwa mbali.
