Mwanamuziki nguli wa Uganda Jose Chameleone alizuru Tanzania juzi katika kile alichokitaja kuwa ziara ya kushukuru mashabiki wake kwa kusimama naye alipougua.
“Ningependa kushukuru watu wa Tanzania kwa maombi na usaidizi wakati nilikuwa nikiugua” aliandika mwanamuziki huyo akiongeza kusema kwamba ukarimu wao na imani vilimuinua sana alipokuwa na mahitaji makubwa.
Chameleone alisema alikwenda Tanzania kuwasilisha shukrani zake binafsi huku akisherehekea uponyaji wake.
Kati ya watu aliokutana nao nchini humo ni rafiki yake wa muda mrefu Profesa Jay ambaye pia aliwahi kuugua kwa muda mrefu baadaye walionekana kwenye studio ya mtayarishaji wa muziki wa Hip Hop nchini Tanzania Bin Laden.
Bin Laden alithibitisha kwamba wawili hao wanaandaa kazi ya muziki ya pamoja.
Wanamuziki hao wamewahi kushirikiana katika muziki kwenye vibao viwili kimoja kiitwacho ‘Ndivyo Sivyo’ cha miaka 11 iliyopita na cha pili ‘Kwa Ajili Yako’ cha miaka kumi iliyopita.