Mwanahabari wa burudani na mtangazaji maarufu nchini Uganda Zahara Totto amesema kwa ujasiri kuwa alibadilisha kabisa namna habari za burudani zinapotiwa nchini humo.
Kulingana naye, mtindo alioanzisha ni wa kipekee na bado unaendelea kuathiri sekta hiyo.
Akizungumza katika mahojiano Zahara alikumbuka safari yake ya utangazaji wa televisheni na kueleza fahari yake kwa mchango anaodai aliacha alipokuwa akiwasilisha habari za burudani.
Kwa mujibu wa mtangazaji huyo anayefahamika kwa kauli zake za wazi, mtindo wake ulikuwa wa kipekee na wa kukumbukwa, jambo lililofanya iwe vigumu kwa mtu mwingine kuiga.
“Hakuna mtangazaji nchini Uganda atakayewahi kuziba nafasi yangu kwa sababu kile nilichofanya kilikuwa cha kukumbukwa,” alisema Zahara Totto akiongeza “Watu Bado Wanaiga Mtindo Wangu”.
Zahara alisema watangazaji wengi wanashindwa kujitofautisha kwa sababu wanajikita katika kuiga namna yake ya uwasilishaji badala ya kujenga utambulisho wao wenyewe.
Alieleza kuwa mtindo wake wa uwasilishaji ni kipaji cha asili ambacho hakiwezi kuigwa rahisi.
“Ni kipaji nilichopatiwa na Mungu. Nilibadilisha namna habari za burudani zinawasilishwa nchini Uganda, na ndiyo maana hata leo unaona watu kwenye TikTok wakijaribu kufanya kwa mtindo huo huo,” aliongeza.