Ibraah adaiwa bilioni moja kabla ya kuondoka Konde Music

Msanii huyo sasa ameanzisha mchango mitandaoni ili kupata pesa za kulipa ada anayodaiwa.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa mtindo wa Bongo Fleva nchini Tanzania Ibrahim Abdallah Nampunga maarufu kama Ibraah amesema kwamba ametakiwa kulipa shilingi bilioni moja pesa za Tanzania ndipo aweze kuondoka kwenye kampuni ya Konde Music.

Kampuni ya Konde Music au ukipenda Konde Gang inamilikiwa na mwanamuziki Harmonize.

Kupitia Insta Stories, Ibraah aliomba watanzania usaidizi akisema, “Dah! hili limenishinda narudi kwenu kama watanzania mzee Konde anataka nimlipe bilioni moja.”

Ibraah alishangaa kiasi cha pesa anachoitishwa na mkubwa wake akisema kwamba tangu aanze kazi kama mwanamuziki hajawahi kujipatia hata robo ya bilioni.

Msanii huyo kisha aliendela kwa kuomba usaidizi wa kifedha kutoka kwa watanzania wenza ili aweze kulipa kiasi anachodaiwa cha pesa ndiposa apate uhuru kutoka Konde Gang.

Alitoa nambari ya kutuma pesa kwenye tangazo hilo.

Kampuni ya Konde Music haijatoa taarifa rasmi kuhusu madai ya Ibraah lakini siku nne zilizopita, video ya wimbo wake mpya uitwao ‘Copy and Paste’ ilichapishwa kwenye ukurasa wa Instagram wa kampuni hiyo.

Kando na Harmonize, Ibraah ndiye msanii wa pekee kwenye kampuni hiyo ya Konde Music baada ya wasanii wa awali kama Cheed, Killy na Anjella kuondoka.

Inadaiwa kwamba mikataba yao ilisitishwa ghafla na kwamba walikuwa wananyanyaswa na usimamizi wa kampuni hiyo.

Visa vya kampuni za muziki kuitisha pesa nyingi kwa wasajiliwa wanaotaka kuondoka sio jambo geni nchini Tanzania, Harmonize na Rayvanny walikabiliwa na hali sawia walipokuwa wakiondoka Wasafi Music inayomilikiwa na Diamond Platnumz.

Mbosso hata hivyo aliondoka Wasafi bila malipo hivi maajuzi ambapo Diamond alielezea kwamba ni kwa sababu ya heshima iliyodumu kati yao.

Website |  + posts
Share This Article