Mwanamuziki wa Tanzania Rajab Abdul Kahali maarufu kama Harmonize na Fridah Kajala wameonyesha hadharani kwamba wamerudiana kama wapenzi.
Hili lilidhihirika katika hafla ya kifahari iliyoandaliwa kwa ajili ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya mjukuu wa Kajala aitwaye Amara ambaye ametimiza umri wa mwaka mmoja.
Hafla hiyo ilipeperushwa moja kwa moja na runinga ya Clouds ambapo Kajala na Harmonize walionekana wakiwa wameketi kwenye meza moja, wakiwa wamevaa mavazi ya rangi nyeupe.
Alipopatiwa fursa ya kutumbuiza, Harmonize aliimba pamoja na Kajala huku Paula binti ya Kajala na Marioo ambao ni wazazi wa mtoto Amara wakicheza nao.
Katika hotuba yake, Harmonize alisema anafahamu furaha ya kuwa na mtoto huku akihimiza wazazi waendelee kumlea Amara vyema hata ingawa anaelewa kazi ya Marioo ya muziki huwa inachukua muda wake mwingi.
Kajala alimpongeza binti yake kwa kuwa mama bora akisema kwamba kwa mwaka mmoja amekuwa akimfuatilia hajaona akiwa na mchezo na mtoto wake.
Mtangazaji wa Kenya Azeezah Hashim ndiye alikuwa mwongoza sherehe na sasa anaonekana kupendelewa na watanzania baada ya kutimiza jukumu sawia katika harusi ya Hamisa Mobetto.
Baba mzazi wa Paula P Funk naye alikuwepo na alishukuru Mungu kwa afya ya mjukuu wake huku akisifia pendo lililopo kati ya Paula na Marioo akisema hajawahi kuambiwa kuhusu kutoelewana kati yao.
Awali, Mwijaku aliwahi kutangaza kurudiana kati ya Harmonize na Kajala kiasi cha eneo la tukio kuandaliwa lakini hakuna hafla iliyofanyika. Sasa inasubiriwa kuona iwapo wataandaa hafla rasmi ya kutangaza kwamba wamerudiana.