Mwanamuziki wa Tanzania Abdul Naseeb maarufu kama Diamond Platnumz amefafanua kuhusu kuondoka kwa msanii mwenza Mbosso Khan kwenye kampuni ya Wasafi.
Diamond ambaye ni mkurugenzi na mwanzilishi wa kampuni hiyo ya Wasafi alikuwa akizungumza na wanahabari katika mkutano mkuu wa chama tawala cha CCM jijini Dodoma wa kuadhimisha miaka 48 tangu kilipoasisiwa.
Alisema kwamba Mbosso alimwomba aondoke akajisimamie kama msanii huru na kwamba alikuwa tayari kulipa fedha kabla ya kuondoka kulingana na masharti na taratibu za kampuni.
Msanii huyo anasema hakumtoza Mbosso hata shilingi kumi kwa sababu ya hekima, heshima na mapenzi yake kwake.
“Wiki mbili nyuma tuliongea na Mbosso na aliniomba aanze kujisimamia na nimempa baraka zote na Mbosso ni Mdogo wangu, sababu ya kumsajili Mbosso nilikuwa nampenda, mimi na Mbosso hatujawahi kugombana.” alisema Diamond.
Platnumz aliendelea kufsema kwamba tayari mchakato mzima wa Mbosso kuondoka Wasafi umekamilika na alikuwa Dodoma kama msanii huru.
Aliahidi kuendelea kumuunga mkono Mbosso ambaye anasema ataendelea kuwa mwanafamilia ya Wasafi.
Habari za kuondoka kwa Mbosso kwenye kampuni ya Wasafi zilifichuliwa na Baba Levo mtangazaji wa kituo cha redio cha Wasafi Fm kupitia Instagram.
Baba Levo alifichua pia kwamba kampuni hiyo inapanga kusajili wasanii kadhaa wapya mwaka huu wa 2025.