Kenya yaadhimisha siku ya kimataifa ya kutokomeza ukeketaji wa wanawake

Ann Wang'ombe, ambaye ni katibu wa idara ya jinsia na ustawi wa jamii, alipongeza juhudi za Kenya, akisema kiwango cha ukeketaji kilipungua kutoka asilimia 21 mwaka 2014 hadi asilimia 15 mwaka 2022.

Marion Bosire
2 Min Read

Leo Februari 6, 2025, ulimwengu unaadhimisha siku ya kimataifa ya kutokomeza ukeketaji wa wanawake ambapo Kenya ilionyesha mafanikio yake makubwa katika kupambana na utamaduni huo.

Akizungumza katika kaunti ya Meru, Ann Wang’ombe, ambaye ni Katibu wa Idara ya Jinsia na Ustawi wa Jamii alipongeza juhudi za Kenya, akisema kuwa kiwango cha ukeketaji huo kilipungua kutoka asilimia 21 mwaka 2014 hadi asilimia 15 mwaka 2022.

Wang’ombe alionyesha matumaini kwamba tafiti zijazo zitadhihirisha upungufu zaidi, lakini alionya kuhusu kurejea kwa visa vya ukeketaji katika eneo la kati mwa nchi.

Alisisitiza kwamba serikali haitakoma kupambana na ukeketaji.

Katibu huyo pia alishukuru serikali kwa msaada wake unaoendelea, hasa kwa uungwaji mkono kutoka kwa Rais William Ruto katika kushughulikia mauaji ya wanawake na dhuluma za kijinsia.

Alisisitiza kuhusu kuanzishwa kwa kikosi kazi kitakachoshughulikia masuala haya.

Aurelia Rono, Katibu wa Masuala ya bunge alirejelea kauli za Wang’ombe, akisema kwamba bodi ya kukabiliana na ukeketaji itaendelea na juhudi zake za kuelimisha na kuhamasisha umma kuhusu hatari za ukeketaji na dhuluma za kijinsia.

Gavana wa kaunti ya Meru Kawira Mwangaza alitoa shukrani kwa maandalizi ya hafla ya kitaifa ya siku ya ulimwengu ya kutokomeza ukeketaji wa wanawake katika kaunti yake, akishukuru makatibu hao wawili na wenzao kwa kujitolea kwao katika kupambana na ukeketaji.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *