Miaka 50 ya kipindi cha SNL

Awamu ya 50 ya kipindi hicho kilichoanzishwa mwaka 1975 inaangazia kumbukumbu za vipindi vya awali.

Marion Bosire
2 Min Read

Kipindi cha Saturday Night Live cha Marekani almaarufu SNL kinaadhimisha miaka 50 tangu kilipoanzishwa.

SNL kilianzishwa rasmi Oktoba 11, 1975 na tangu wakati huo kimekuwa muhimu katika utamaduni wa Marekani na kinaangaziwa sana na wachekeshaji na hata utamaduni wa pop.

Kipindi hicho cha mahojiano kimehusisha wachekeshaji, waigizaji na wanamuziki mbali mbali katika uwepo wake, huku kikiacha picha isiyosahaulika katika akili za watazamaji.

Tangu siku za Chevy Chase, John Belushi na Gilda Radner, hadi kwa nyota wa hivi punde zaidi kama Kristen Wiig, Kate McKinnon na Pete Davidson, kipindi cha SNL kimekuwa kikikiuka mitindo ya kawaida.

Huwa kinahusisha dhihaka za kisiasa, mitindo ya kijamii na wahusika wa tasnia ya uigizaji huko Hollywood.

Awamu hii ya 50 inahusisha kumbukumbu za vipindi vya awali na katika mojawapo ya kumbukumbu hizo, mwanamuziki R. Kelly aliangaziwa.

Katika kitengo hicho cha kumbukumbu, wageni wa awali ambao walikuwa wasumbufu waliangaziwa na R. Kelly akawa mmoja wao pamoja na Diddy, O.J Simpson, Jared Fogle na Robert Blake.

Wakili wa Kelly ameghadhabishwa na hatua hiyo akisema kwamba hatua hiyo ni ya kiburi kwamba SNL ndiyo inaamua anayefanikiwa na anayesusiwa katika kazi kama muziki na uigizaji.

Wakili huyo kwa jina Jennifer Bonjean, aliongeza kusema kwamba anajua wageni wengine wengi wa awali ambao walikuwa wasumbufu na hawakujumuishwa kwenye orodha ya SNL.

R. Kelly kwa sasa yuko jela ambako anatumikia kifungo cha pamoja cha miaka 31. Mwaka 2021,alihukumiwa kifungo cha miaka 30 gerezani kwa makosa ya ulanguzi wa binadamu kwa ajili ya kuwatumia kingono huko New York.

Mwaka 2023, alipokea hukumu nyingine ya miaka 20 gerezani huko Chicago kwa kutumia watoto kutengeneza maudhui ya kingono na kuvutia watoto kingono.

Miaka 19 ya kifungo hicho anaitumikia kwa pamoja na kifungo cha awali kisha baadaye atumikie mwaka mmoja utakaokuwa umesalia na hivyo atakuwa huru kuanzia Disemba 2045.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *