Mwigizaji wa Nigeria Chika Ike amevunja kimya kuhusu uvumi ambao umekuwa ukienea mitandaoni kumhusu.
Chika alichapisha picha zake za ujauzito mitandaoni na ghafla akaangaziwa sana ndani na nje ya Nigeria wengi wakikisia baba ya mtoto wake na hali yake inavyohusiana na mwigizaji mwenza Regina Daniels.
Leo, amechapisha picha nyingine inayomwonyesha akiwa mjamzito na kuandika, “Kumekuwa na uongo wa kila aina unaosambazwa kunihusu kwenye vyombo vya habari kwa miaka kadhaa, lakini nikauchukulia ulivyokuwa, uvumi ambao haukuhitaji jibu.”
Binti huyo aliendelea kwa kusema kwamba zamu hii mambo ni tofauti kwani yanahusu mwanawe kwani hakuna anayejua lolote kumhusu.
Alisema yeye ni msiri mno hakuna anayeweza kujua lolote hadi yeye mwenyewe afichue yanayoendelea maishani mwake.
“Ned sio baba ya mwanangu na jina lolote mtakaloibuka nalo baadaye mnapokisia na nilivyosema awali mimi sio mke wa saba wa mtu! Ndoa ya wake wengi sio mtindo wangu.” aliandika Chike na hivyo kulaza uvumi ambao umekuwa ukiendelea kusambaa.
Haya yanafuatia hatua ya Regina Daniels ya kuficha akaunti yake ya Instagram baada ya kusalia kimya katika siku ya wapendanao Februari 14, 2025, kinyume na awali.
Baadaye Chika alipochapisha picha zake za ujauzito, wanamitandao wa Nigeria wakaanza kukisia kwamba huenda baba ya mtoto ni Ned Nwoko ambaye ni mume wa Regina Daniels, ndiposa akakasirika kiasi cha kujiondoa mitandaoni kwa muda.
Chika anasema anaelewa uvumi unafuata kutokana na tasnia aliyochagua ya uigizaji na sababu pekee ya kujibu uvumi wa hivi punde zaidi ni kwamba unahusu mwanawe.
“Usiri wangu ndio amani yangu na kamwe hakuna atakayenitikisa. Ninafurahikia ujauzito wangu kwa sasa na muda huu hilo pekee ndilo la muhimu.” alimalizia Chika.