Zawadi ya gari kwa baba mkwe

Bahati alichagua hiyo kuwa zawadi ya kwanza kwa mkewe Diana Bahati wanapoadhimisha miaka minane ya ndoa.

Marion Bosire
1 Min Read

Kevin Bahati ambaye ni mwanamuziki alimzawadi baba ya mke wake Diana gari jipya, hiyo ikiwa zawadi ya kwanza kati ya zawadi nane alizoahidi kumpa mkewe wanapoadhimisha miaka minane ya ndoa.

Katika video iliyochapishwa mitandaoni, Bahati alisimulia jinsi ilikuwa vigumu kumshawishi baba mkwe aje nyumbani kwao kwa ajili ya kupokea zawadi huku akitaka isalie kuwa jambo la kushtukizia.

Bahati ambaye awali alikuwa amemzawadi Diana shilingi milioni nane alikuwa ameweka zawadi hiyo ya gari kuwa siri kwa wanafamilia wote.

Babake Diana naye hakujua alichoitiwa.

Giza lilipoingia Bahati alifika nyumbani akiwa na zawadi hiyo ya gari, akaiacha mbali kidogo akaingia kwenye nyumba akamwita mzee na wakafuatwa na wengine akiwemo Diana na dada zake.

Mzee huyo ambaye Bahati alimrejelea kuwa baba mkwe bora zaidi ulimwenguni alifurahikia zawadi yake, akawa mwingi wa shukrani huku akiahidi kuendelea kuwa baba bora.

Diana alifurahikia zawadi yake ya kwanza ambayo aliirejelea kuwa fursa ya kumwona babake akiwa amefurahi. Alisema Bahati alipitia mengi lakini akachagua kuwa baraka kwa babake.

“Umekuwa mwana wa kiume ambaye baba hakufanikiwa kupata. Umemfanya Mungu atabasamu, umewafanya wazazi wako watabasamu waliko mbinguni. Umenifurahisha.” aliandika Diana.

Sasa inasubiriwa kuona ni zawadi gani alizompangia Bahati hadi zifike nane.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *