Mwigizaji wa Tanzania Carina afariki

Mwigizaji huyo amefariki akiendelea kupokea matibabu nchini India kutokana na maradhi ya tumbo yaliyomsibu kwa muda mrefu.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwigizaji wa Tanzania Hawa Hussein Ibrahim maarufu kama Carina ameaga dunia leo Aprili 15,2025 akiendelea kupokea matibabu nchini India kutokana na maradhi ya tumbo yaliyokuwa yakimsumbua kwa muda wa zaidi ya miaka minane.

Taarifa hizo zimethibitishwa na mdogo wake Safinewin Rwegasira ambaye alienda naye India lakini akarejea kwa ajili ya kumtunza mama yao ambaye pia ni mgonjwa.

Safinewin ameelezea kwamba mara ya mwisho kuongea na dadake ni usiku wa kuamkia leo na alikuwa katika hali nzuri tu huku akiahidi mama yao kwamba hatamani kufariki na anatamani kurejea akiwa mzima ili aweze kutimiza yale aliyoahidi.

“Nimeongea nae, alikuwa yuko vizuri tu dada yangu akawa anaongea na Mama anamwambia naomba Mungu nisife kabla yako, sijatimiza ahadi zangu zote nilizokuahidi” alisema Safinewin akiongeza kwamba tayati alikuwa amekamilisha upasuaji na angerejea Tanzania Aprili 22, 2025.

Carina alisafiri kuelekea India Februari 24, 2025 baada ya kufanikiwa kuchangisha pesa ambazo alikuwa anahitaji kwa ajili ya matibabu ambazo ni shilingi milioni 54 pesa za Tanzania.

Alifanyiwa upasuaji mara 24 kujaribu kusuluhisha matatizo yake ya tumbo bila mafanikio.

Kando na uigizaji kwenye filamu za Bongo, Carina aliwahi kuhusika katika video ya wimbo Oyoyo wa mwanamuziki Bob Junior.

Website |  + posts
Share This Article