Maafisa wa Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi EACC, wamemkamata Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi, kwa madai ya kushiriki ufisadi.
Kulingana na EACC, maafisa wengine tisa wa kaunti hiyo pia walikamatwa kwenye operesheni hiyo, wanaodaiwa walihusika katika ubadhirifu wa pesa za umma na ukinzano wa maslahi katika maswala ya ununuzi.
Tisa hao ni pamoja na Peter Njoroge Ndegwa mbaye ni katibu wa kaunti, Nancy Njeri Kirumba(Waziri wa Fedha), Salome Muthoni Wainaina(Waziri wa Ardhi), William Kinyanjui Kimani(Afisa Mkuu wa Fedha), Phylis Wanjiru Muiruri, Henry Mburu Waweru(Mkurugenzi wa mapato), Paul Kibe Wangari na Bernard Kabaiku Theuri.
Maafisa hao wa EACC, walivamia makazi ya Gavana huyo na afisi za kaunti hiyo, ambapo walichukua baadhi ya stakabadhi na vifaa vya elektroniki.
Washukiwa hao wanatarajiwa kuandikisha taarifa katika afisi za EACC.
Mnamo mwezi Febuari mwaka huu, Seneta wa Kiambu Karungo Wa Thang’wa alitoa wito kwa tume hiyo kuchunguza madai ya wafanyakazi hewa na ubadhirifu wa shilingi milioni 390.