Siku ya Kiswahili Duniani kuadhimishwa leo

Kaulimbiu ya mwaka huu ni "Kiswahili kwa Amani, Mshikamano na Diplomasia ya Uchumi wa Kimataifa".

Marion Bosire
2 Min Read

Dunia leo inaadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani, inayojiri tarehe 7 Julai, kila mwaka huku lugha ya Kiswahili ikiendelea kutambuliwa kama nyenzo muhimu ya kuimarisha amani, umoja na maendeleo endelevu.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Kiswahili kwa Amani, Mshikamano na Diplomasia ya Uchumi wa Kimataifa,” ikisisitiza nafasi inayozidi kukua ya Kiswahili katika kukuza mazungumzo kati ya tamaduni mbalimbali, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuendeleza ushirikiano wa kimataifa.

Maadhimisho makubwa ya dunia yanafanyika katika makao makuu ya shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO jijini Paris, nchini Ufaransa.

Humu nchini Kenya maadhimisho yanaandaliwa katika chuo kikuu cha Kenyatta kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa nane mchana, huku hafla hiyo ikipeperushwa mubashara na runinga ya KBC Channel 1.

Shirika la utangazaji nchini KBC limetoa mchango mkubwa katika kuendeleza lugha ya Kiswahili kupitia kituo cha redio cha KBC Radio Taifa ambacho hurusha matangazo yake kwa Kiswahili.

Vipindi vya ‘Sanaa ya Kiswahili’ cha runinga na ‘Ramani ya Kiswahili’ pia vina umuhimu mkubwa kwani wasikilizaji na watazamaji hupata kunoa makali ya lugha hiyo huku wakipata burudani.

Jijini Bujumbura, nchini Burundi, kuna hafla nyingine ya maadhimisho hayo itakayokutanisha wadau wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC.

Hii ni awamu ya tano ya maadhimisho hayo katika EAC na ya tatu kwa Tume ya Kiswahili ya Afrika Mashariki.

Washiriki wanajadili matumizi ya lugha nyingi na namna ya kuingiza Kiswahili katika teknolojia ibuka, ikiwemo Akili Unde ili kukifanya kiendelee kustawi katika enzi ya kidijitali.

Share This Article