Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS siku ya Jumapili imefanya mabadiliko kwenye kitengo cha maafisa wa polisi wa kumlinda Rais.
Mabadiliko hayo yanajiri saa chache baada ya agizo la Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja kufuatia tukio lililokiuka utaratibu wa usalama wa Rais katika eneo la Ganze, kaunti ya Kilifi.
Kwenye mabadiliko hayo yaliyotiwa saini na Naibu Inspekta Mkuu wa Polisi Eliud Lagat, William Sawe kutoka kitengo cha Recce, ameteuliwa Kamanda wa kitengo cha ulinzi wa Rais, huku aliyekuwa Kamanda wa kitengo hicho Noah Kirwa Maiyo, akihamishwa hadi Makao Makuu ya Polisi.
Naibu Kamanda wa kitengo hicho Juda Mathews Gwiyo, amepewa likizo akisubiri muda wa kustaafu, wadhifa wake ukichukuliwa na George Kirera.
Huku akilaani tukio hilo la Ganze, Kanja amesema usalama wa kiongozi wa taifa ni suala la usalama wa taifa na unapaswa kushughulikiwa kwa umakini wa hali ya juu.
Aliwaonya wananchi dhidi ya kukiuka taratibu zilizopo za usalama wa Rais, akisema NPS itahakikisha suala kama hilo halitokei tena katika siku za usoni.