Marehemu Wakili Mkuu Pheroze Nowrojee amekumbukwa kupitia kwa kuipa barabara moja ya Nairobi jina lake.
Barabara ya Galana katika mtaa wa Kilimani, kaunti ya Nairobi sasa inaitwa “Pheroze Nowrojee Road” kama njia ya kuendeleza urithi wa wakili huyo katika jiji alilohudumia kisheria.
Hafla ya kubadili jina la barabara hiyo iliandaliwa jana Mei 4, 2026 na ilihudhuriwa na watu wa familia yake, wanaharakati na viongozi kadhaa hasa wa tasnia ya sheria nchini.
Wanasheria hao walionekana kufurahia utambuzi huo wa wakili mwenza aliyepigania haki, haki za binadamu pamoja na demokrasia.
Wakili Mkuu Martha Karua alisema kwamba hafla ya jana ilikuwa hitimisho la safari iliyoanza mwaka jana inayowakilisha utahimilivi na ujasiri wa Marehemu Nowrojee.
“Kwamba hata ingawa kulikuwa na changamoto za hapa na pale, zilizojitokeza hakuna kurudi nyuma na tuko hapa sasa kwa ajili ya kuzindua ,” alisema Karua huku akishukuru mkewe Nowrojee na familia yake kwa kumtoa kwa wakenya.
Huku wakishangiliwa na kupigiwa makofi Karua pamoja na mkewe Nowrojee aitwaye Viloo waliondoa kitambaa kilichokuwa kimefunika bamba hilo na hivyo kuzindua rasmi jina jipya la barabara hiyo.
Mwanaharakati Boniface Mwangi alitaja hatua hiyo ya kusimika bamba jipya la jina la barabara hiyo kuwa kipekee na kwamba marehemu Nowrojee sasa atakumbukwa milele hata nje ya tasnia ya uanasheria.
Pheroze Nowrojee alifariki Aprili 5, 2025, akiwa na umri wa miaka 84. Aliidhinishwa kuwa wakili nchini Kenya mwaka 1967, baada ya kuidhinishwa kuwa wakili huko London mwaka 1965.
Alikuwa wakili mwenye haiba yake ambaye alikuwa na kibali cha kuhudumu nchini Tanzania, Uganda na hata Ushelisheli.
Kando na kuwakilisha watu mahakamani, aliwahi kuwa mhadhiri katika chuo kikuu cha Nairobi na taasisi ya sheria nchini, KSL.
Pheroze aliokuwa pia mwandishi wa vitabu aliyeandika vitabu vinne ambavyo ni, Pio Gama Pinto: Patriot for Social Justice, A Vote for Kenya: The Elections and the Constitution, A Kenyan Journey na Conserving the Intangible.