Jubilee yakosoa mashambulizi ya kisiasa dhidi ya kiongozi wake

Viongozi wa chama hicho wanasema Rais mstaafu Uhuru Kenyatta anatekeleza haki yake ya kikatiba ya kutoa maoni kuhusu masuala ya kitaifa

Marion Bosire
1 Min Read

Chama cha Jubilee kimekosoa kile kinachokitaja kuwa mashambulizi ya kisiasa yanayoendelea dhidi ya aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta, ambaye pia ni kiongozi wa chama hicho.

Kulingana na chama hicho, mashambulizi hayo yanatekelezwa na baadhi ya viongozi wanaounga mkono serikali pana, kikionya kwamba vitendo hivyo vinaashiria kupungua kwa nafasi ya demokrasia na kutovumilia maoni mbadala.

Akizungumza na wanahabari jijini Nairobi, Naibu Kiongozi wa Chama cha Jubilee, Fred Matiang’i, alieleza kuwa rais huyo wa zamani anatekeleza haki yake ya kikatiba ya kutoa maoni kuhusu masuala ya kitaifa na hivyo hapaswi kutishwa.

Matiang’i alikuwa ameandamana na viongozi wakuu wa chama cha Jubilee waliosema kwamba mashambulizi dhidi ya rais huyo wa zamani yanadhihirisha kwamba walio mamlakani hawaridhii sauti mbadala katika uwanja wa demokrasia nchini.

Viongozi hao pia walikosoa madai ya vitisho vya kuondoa marupurupu ya serikali yanayotolewa kwa rais mstaafu, wakisema hatua hiyo ni kinyume cha katiba na ina misukumo ya kisiasa.

Wakati huo huo, viongozi wa Jubilee walipinga mipango ya serikali ya kuanzisha ushuru unaolenga biashara ya mitumba, wakisema mapendekezo hayo yanaweza kuwa mzigo kwa wafanyabiashara wadogo na maelfu ya Wakenya wanaotegemea sekta hiyo kujipatia riziki.

Share This Article