Mudavadi: Maandalizi ya ziara ya Rais Ruto nchini Italia yanendelea

Ziara hiyo ya kiserikali inalenga kupanua mazungumzo kati ya sekta tofauti ikiwa ni pamoja na sekta ya maji, utalii, uchumi wa kidijitali, nishati, kilimo, afya na leba.

Tom Mathinji
1 Min Read
Mkutano kuhusu ziara ya Rais William Ruto nchini Italia waandaliwa.

Waziri Mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, amesema kuwa maandalizi ya ziara ya Rais William Ruto nchini Italia yameshika kasi.

Mudavadi, ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, alisema amepokea habari za kina kutoka maafisa wakuu wa wizara hiyo kuhusu mipango ya ziara hiyo.

Kulingana na Mudavadi, ziara hiyo ya kiserikali inalenga kupanua mazungumzo kati ya sekta tofauti ikiwa ni pamoja na sekta ya maji, utalii, uchumi wa kidijitali, nishati, kilimo, afya na leba.

Aidha, mazungumzo hayo yataangazia ufanisi ulioafikiwa tangu Rais wa Italia Sergio Mattarella alipozuru Kenya mwaka 2023, huku nchi hizo mbili zikilenga kuimarisha uhusiano wao wa kidiplomasia na kiuchumi.

Wakati huo huo, Mudavadi alisema maandalizi yanaendelea kuhusu ziara ya Waziri wa Mambo ya nje wa Portugal Paulo Rangel hapa nchini

“Nilipokea ripoti kuhusu ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Portugal Paulo Rangel hapa nchini, ambaye nitashiriki naye meza ya mazungumzo kuhusu kuboreshwa kwa ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi, kabla yake kushauriana na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi,” alisema Mudavadi.

Alidokeza kuwa sera ya Kenya kuhusu maswala ya kimataifa, inaendelea kubuni ushirikiano unaopanua fursa za kiuchumi na kuwafaidi wananchi.

Share This Article