Bunduki mbili zasalimishwa kwa polisi Isiolo

Tom Mathinji
1 Min Read
Bunduki mbili zasalimishwa kwa polisi Isiolo.

Bunduki mbili haramu zimesalimishwa kwa maafisa wa polisi katika kaunti ya Isiolo, katika sehemu ya operesheni ya kiusalama inayoendelea almaarufu ‘Operation Dumisha Usalama’.

Kulingana na Huduma ya Taifa ya Polisi, silaha hizo, bunduki aina ya AK-47 na bunduki aina ya G3, zilisalimishwa kwa hiari siku ya Jumatatu Aprili 13, 2026 kutoka kwa wakazi wawili wa eneo la Lowangila, kaunti ndogo ya Isiolo Kaskazini.

Polisi wamesema bunduki hizo pamoja na risasi, zinahifadhiwa katika kituo cha polisi, huku utawala ukiendelea kuchukua hatua zaidi.

“Huduma ya Taifa ya Polisi inawapongeza wananchi kwa ushirikiano wao kwenye operesheni hiyo ya kiusalama,” ilisema Huduma ya Taifa ya polisi.

Aidha, huduma hiyo ilidokeza kuwa bunduki hizo zilisalimishwa kutokana na ushirikiano wa wananchi kwenye operesheni inayoendelea inayolenga bunduki haramu na kurejesha usalama katika eneo hilo.

Maafisa wa Polisi wametoa wito kwa watu ambao bado wanamiliki silaha haramu, kuchukua fursa hii ya kipindi cha msamaha kuzisalimisha katika kituo cha polisi kilicho karibu.

TAGGED:
Share This Article