Idadi ya wanaofariki kutokana na Ebola yaendelea kuongezeka DRC

Tom Mathinji
1 Min Read
Idadi ya wanaofariki kutokana na Ebola yazidi kuongezeka.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema takriban watu 139 wamefariki kutokana na maambukizi ya ugonjwa wa Ebola, huku visa 600 vya ugonjwa huo vikiripotiwa.

Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, visa 51 vimethibitishwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), huku visa viwili vikinakiliwa katika taifa jirani la Uganda.

Akizungumza na wanahabari Jijini Geneva nchini Uswizi,  Ghebreyesus alisema mlipuko wa ugonjwa wa Ebola aina ya Bundibugyo huenda ulitokea miezi michache iliyopita.

Mnamo siku ya Jumapili, WHO ilitangaza afya ya umma kuwa dharura ya kimataifa, lakini ikadokeza kuwa haijafika kuwa kiwango cha janga.

“WHO inakadiria hatari ya ugonjwa huo kuwa ya juu katika kiwango cha taifa na kikanda, lakini ya chini katika kiwango cha kimataifa,” alisema mkurugenzi huyo.

Visa hivyo 51 vya Ebola nchini DRC vimenakiliwa katika mkoa wa Mashariki wa Ituri na katika mkoa wa Kaskazini wa Kivu, huku visa viwili nchini Uganda vikinakiliwa Jijini Kampala.

Share This Article