Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, siku ya Jumatano amewateua Majaji wa Mahakama ya Rufaa, hatua inayoashiria lengo la kuimarisha Mahakama ya Rufaa katika taifa hilo la Afrika Mashariki.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Bakari Machumu, walioteuliwa wanajumuisha Majaji wa Mahakama za Juu kutoka eneo lote la nchi hiyo.
Walioteuliwa ni Jaji Abdi Shaban Kagomba wa Mahakama Kuu ya Dodoma, Jaji Yohane Bokobora Masara wa Mahakama Kuu Arusha, na Jaji Immaculata Kajetan Banzi wa Mahakama Kuu ya Kagera.
Wengine ni Jaji Rabia hussein Mohamed wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Jaji Cyprian Phocas Mkeha wa Mahakama Kuu ya kushughulikia kesi za kiuchumi Dar es Salaam, na Jaji Yose Joseph Mlyambina Jaji wa Mahakama Kuu ya kushughulikia kesi za wafanyakazi Dar es Salaam.
Kwenye orodha hiyo pia inajumuisha Jaji Imani Daud Aboud wa Mahakama Kuu ya Dodoma, Jaji Mzee Ibrahim Ibrahim wa Mahakama Kuu ya Zanzibar na Jaji laurent Masabo Jaji Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Dodoma.
Taarifa hiyo imesema kuwa tarehe ya kuwaapisha majaji hao wateule itatangazwa baadaye.