Kesi ya uhaini inayomkabili Lissu yaahirishwa

Hakimu Mfawidhi Franko Kiswaga ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 19, 2025 huku akiutaka Upande wa serikali kukamilisha upelelezi.

Marion Bosire
2 Min Read
Kiongozi wa chama cha CHADEMA Tundu Lissu

Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, jijini Dar es Salaam imeahirisha kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu.

Katika kikao cha kutaja kesi hiyo leo,Mei 6, 2025, mbele ya Hakimu Mfawidhi, Franko Kiswaga ilibainika kwamba upande wa serikali haujakamilisha upelelezi katika kesi hiyo ya uhaini dhidi ya mwenyekiti wa CHADEMA.

Hakimu Kiswaga ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 19, 2025 huku akiutaka Upande wa serikali kukamilisha upelelezi.

Wakili wa Serikali Tawabu Issa aliambia mahakama kwamba shauri limekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi haujakamilika. Alitaja pia hatua ya mshtakiwa kugoma kushiriki kesi hiyo kwa njia ya mtandao kutoka gereza la Ukonga.

Msimamizi mkuu wa gereza la Ukonga Juma Mwaibako amedai kwamba Tundu Lissu amekataa kusikiliza shauri hilo kwa njia ya mtandao.

Madai ya kutokamilika kwa upelelezi yalipingwa vikali na mawakili wa utetezi wakiongozwa na Mpale Mpoki aliyesema kwamba haoni sababu ya upelelezi kutokamilika kwa muda wa takribani siku 27.

Akiwa nje ya mahakama, wakili Rugemeleza Nshala ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa chama cha upinzani CHADEMA ameelezea kuhusu mwenendo wa shauri hilo na kusema wanataka kuona upelelezi ukikamilika haraka.

Lissu alifikishwa kwenye mahakama hiyo kwa mara ya kwanza Aprili 10, 2025 akikabiliwa na kesi mbili za jinai moja ya uhaini na ya pili ya kuchapisha taarifa za uongo ambayo alisomewa mbele ya Mahakimu wawili tofauti.

Website |  + posts
Share This Article