Kenya imeweka hatua za kimakusudi za kuimarisha uwezo wake wa kitaifa wa akili unde, AI wakati ikikuza ubunifu na kujifunza kutoka kwa nchi zilizoendelea katika nyanja hiyo duniani.
Hayo yamesemwa na Rais William Ruto wakati alipozuru kituo cha Alem.AI Centre jijini Astana nchini Kazakhstan.
Ruto ambaye yuko kwenye ziara ya siku mbili nchini humo alitembelea kituo hicho ili kujionea hatua kubwa zinazofanywa kituoni hapo kuendeleza akili unde na ubunifu wa kidijitali.
Ameielezea AI kama kitovu cha mabadiliko duniani ikichochea ubunifu na fursa mpya za ukuaji uchumi katika kila sekta.

Wakati huohuo, kiongozi wa nchi amesema Kenya imedhamiria kuimarisha biashara na kupanua fursa za kiuchumi na Kazakhstan kwa ajili ya ustawi wa pamoja kati ya nchi hizo mbili.
Ili kukuza uhusiano kati ya nchi hizo, Ruto amesema wanapania kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kati ya Nairobi na Astana ili kuwezesha biashara na kuhamasisha ushirikiano mkubwa wa watu hadi watu.
Aliyasema hayo alipohutubia Kongamano la Kibiashara kati ya Kazakhstan na Kenya katika Kituo cha Kimataifa cha Fedha cha Astana akiwa ameandamana na mwenyeji wake Rais Kassym-Jomart Tokayev.
