Murkomen: Kitengo cha polisi wa Nairobi kitafanikisha uzingatiaji sheria

Tom Mathinji
1 Min Read
Murkomen asifu hatua zilizopigwa katika kubuni kitengo cha maafisa wa polisi wa Jiji la Nairobi.

Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, amepongeza hatua zilizopigwa katika kubuni kitengo cha maafisa wa polisi wa Jiji la Nairobi.

Kulingana na Murkomen, kitengo hicho, kitaimarisha usalama na uzingatiaji wa sheria Jijini Nairobi na maeneo ya karibu.

“Nimefurahishwa kwamba kundi la kiufundi limejifunza mengi kutoka kwa vitengo vya polisi wa jiji kote duniani hususan kuhusiana na ngazi za uongozi pamoja na mikakati ya utendakazi,’ alisema Murkomen.

Aliyasema hayo Jumatano alipopokea ripoti kuhusu hatua zilizopigwa na kamati ya kiufundi inayoshugulikia kubuniwa kwa kitengo hicho cha polisi.

Mkutano huo uliwaleta pamoja Katibu wa ushirikishi wa Serikali ya Taifa Ahmed Abdisalan, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, na  wawakilishi wa serikali ya kaunti ya Nairobi miongoni mwa maafisa wakuu serikalini.

“Kitengo hicho kitaimarisha changamoto ibuka za kiusalama, kitaimarisha ushirikiano wa asasi mbali mbali pamoja na kuboresha ushirikiano kati ya polisi na umma,” aliongeza waziri huyo.

Kubuniwa kwa kitengo hicho kunafuatia ushirikiano kati ya serikali ya taifa na ile ya Jiji la Nairobi, kuhakikisha usalama wa wakazi, wageni na wawekezaji wa jiji hilo.

Share This Article