Operesheni ya pamoja iliyotekelezwa na jeshi la Uganda (UPDF) na lile la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC), imesababisha kuokolewa kwa raia zaidi ya 200, waliokuwa mikononi mwa wapiganaji wa Allied Democratic Forces (ADF), katika kambi ya mto Epulu Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kambi hiyo ilikuwa ikiongozwa na kamanda wa ADF, Ssebagala, anayefahamika pia kama Mzee Mayor.
Kulingana na jeshi la Uganda UPDF, kwenye operesheni hiyo wapiganaji kadhaa wa ADF waliuawa na silaha kadhaa kupatikana.
Akizungumza na raia hao waliookolewa, kamanda wa opresheni hiyo Meja Jenerali Stephen Mugerwa, alisema kikosi cha pamoja cha UPDF na FARDC, kimejitolea kuangamiza mitandao yote ya ADF na kurejesha uzingatiaji sheria.
Aliwahimiza raia hao waliookolewa kushirkiana kwa karibu na vikosi vya usalama.
“Tutahakikisha mmekabidhiwa kwa mamlaka husika, ili muungane tena na familia zenu,” alisema Mugerwa.
Miongoni mwa waliookolewa ni msichana wa umri wa miaka 14 ambaye ndiye mchanga zaidi, huku mkongwe zaidi akiwa mvulana wa umri wa miaka 19.
Walielezea masaibu waliyokumbana nazo walipokuwa mateka, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa chakula, kazi za lazima na adhabu kali kwa kuto-tii sheria za ADF.