Serikali imeboresha uajiri wa Wakenya ughaibuni, asema Rais Ruto

Kiongozi huyo wa Kenya alisema serikali imepiga hatua kubwa katika kulainisha mashirika yanayowatafutia wakenya ajira ughaibuni.

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais wa Kenya William Ruto.

Rais wa Kenya William Ruto amesema serikali imechukua hatua za kisheria dhidi ya mashirika bandia ya kuwaajiri raia wa Kenya ughaibuni.

Kwenye mkutano na wakenya wanaoishi nchini Italia siku ya Jumatatu, kiongozi huyo wa Kenya alisema serikali imepiga hatua kubwa katika kulainisha mashirika yanayowatafutia wakenya ajira ughaibuni.

“Tumelainisha mashirika ya kuwatafutia wakenya ajira ng’ambo, tumechukua hatua dhidi ya mashirika bandia ana kubuni idara ya maswala ya ughaibuni ili kuwahudumia vyema wakenya walio ng’ambo,” alisema Rais Ruto kwenye mkutano huo.

Aidha, Ruto alidokeza kuwa serikali inaendelea kushirikiana na raia wa Kenya ili kuimarisha sera za taifa hilo la Afrika Mashariki na kuwafahamisha wakenya kuhusu mabadiliko nchini humo.

“Kupitia mashauriano haya, tumetekeleza mageuzi ili kukabiliana na changamoto zinazokabili wakenya walio ughaibuni,” aliongeza kiongozi huyo.

Aliwafahamisha wakenya hao kuhusu hatua ambazo zimepigwa nchini humo hasa katika sekta za elimu, kubuni nafasi za ajira, uvumbuzi wa kidijali na maswala ya fedha.

Awali kiongozi huyo wa Kenya alishiriki meza ya mazungumzo na Rais wa Italia Sergio Mattarella, ambapo walijadiliana kuhusu kuimarisha uhusiano baina ya mataifa hayo mawili, hasaa katika sekta muhimu, ikiwa ni pamoja na biashara, uwekezaji, Mabadiliko ya Tabianchi, na ustawi wa miundombinu.

Pia aliweka shada la maua kwenye Kaburi la Wanajeshi Walioangamia huko Piazza Venezia, Roma.

Rais William Ruto yuko katika ziara rasmi nchini Italia.

Share This Article