DCI yawatafuta walioteketeza gari kwenye barabara ya Thika

Tom Mathinji
1 Min Read
DCI inawatafuta washukiwa walioteketeza gari Thika Road.

Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), imeanzisha msako dhidi ya watu walioteketeza gari wakati wa maandamano ya kulalamikia ongezeko la bei ya mafuta kwenye barabara kuu ya Thika siku ya Jumatatu.

Kupitia ukurasa wa X, DCI imesema inachunguza kanda ya video ambayo inaaminika kuwanakili washukiwa wakuu waliohusika katika uteketezaji wa gari hilo aina ya Mazda CX-5.

“Tukio hilo halihatarishi tu maisha, lakini pia lilisababisha uharibifu mkubwa wa mali, na uchunguzi unaendelea,” ilisema DCI kwenye taarifa.

Imetoa wito kwa wananchi kutoa habari kuwahusu washukiwa walionakiliwa kwenye video hiyo kwenye kituo cha polisi kilicho karibu ili kufanikisha kukamatwa kwao.

Wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma walishiriki mgomo siku ya Jumatatu kulalamikia ongezeko la bei ya mafuta, ambapo baadhi ya waandamanaji waliteketeza gari hilo.

“Huduma ya Taifa ya Polisi imejitolea kuhakikisha usalama wa umma, kulinda mali na kuhakikisha wanaogeuza maandamano kuwa matukio ya uhuni wanachukuliwa hatua za kisheria,” iliongeza idara hiyo.

TAGGED:
Share This Article