Mgomo wa magari ya uchukuzi wa umma wafutiliwa mbali

Martin Mwanje
1 Min Read

Viongozi wa vyama vya magari ya uchukuzi wa umma wametangaza kufutilia mbali mgomo wao uliopangwa kurejelewa wiki ijayo ikiwa mazungumzo kati yao na serikali yangekosa kuzaa matunda. 

Viongozi hao walisitisha mgomo huo kwa wiki moja ili kupisha mazungumzo na serikali.

“Tumefutilia mbali mgomo, tulikuwa tumeusitisha lakini tumeufutilia mbali. Hivyo, hatutakuwa na mgomo wiki ijayo, tunaenda kazini,” alisema Albert Karagacha, mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Magari, MOA.

“Sote sisi ni Wakenya na tunataka amani humu nchini, na tunataka kuwa na umoja ili tusonge mbele.”

Wadau wa magari ya uchukuzi wa umma waligoma Jumatatu na Jumanne wiki hii kulalamikia bei za juu za mafuta wanazosema zimelamaza utendaji kazi wao.

Ni hali iliyoilazimu serikali kupunguza dizeli kwa shilingi 10, hatua iliyotajwa na wadau hao kuwa tone lisiloweza kukata kiu.

Na sasa baada ya kukutana na Rais William Ruto jijini Mombasa, viongozi wa vyama hivyo wamesema wameridhika na hatua zinazochukuliwa na serikali kudhibiti hali na hivyo kufutilia mbali mgomo.

 

Share This Article