Maafisa wa polisi wamemkamata mshukiwa anayehusishwa na kueneza semi za chuki kwa umma, kupitia mitandao ya kijamii.
Kulingana na polisi, matamshi hayo ya uchochezi ni tisho kwa mshikamano wa umma na udhabiti wa taifa.
Mshukiwa huyo Evans Onyango Kawala, almaarufu Kidero Jasuba mwenye umri wa miaka 33, alikamatwa katika eneo la mtaani Kayole, kufuatia operesheni iliyotekelezwa na maafisa wa Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI).
Onyango Kawala kwa sasa anazuiliwa kwenye korokoro za polisi, akisubiri kufikishwa mahakamani.
DCI ilitoa onyo kwa umma dhidi ya kutoa au kusambaza semi za chuki ambazo zinachochea ghasia au kuhujumu amani na umoja wa kitaifa.
“Wale watakaopatikana wakitekeleza makosa kama hayo watachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria,” ilisema DCI.