Raia wa Uganda wana kila sababu ya kutabasamu baada ya kupata siku kuu ya kitaifa Jumanne, Mei 12, 2026 ambayo ndiyo siku Rais wa nchi hiyo Yoweri Museveni ataapishwa kuhudumu kwa muhula wake wa saba.
Tangazo kuhusu siku hiyo kuwa likizo ya kitaifa, lilitolewa na Katibu Mkuu wa chama tawala NRM, Richard Todwong, jana Jumanne, Mei 5.
Todwong alisema pia kwamba wanatarajia kuwa na wageni takribani wageni 40,000 siku hiyo, katika Viwanja vya Uhuru vya Kololo.
Wageni hao wanajumuisha wakuu wa nchi 35, wanadiplomasia 30 na wajumbe kutoka harakati za ukombozi kama vyama vya African National Congress cha Afrika Kusini, Chama Cha Mapinduzi cha Tanzania, ZANU–PF cha Zimbabwe, FRELIMO cha Mozambique na Rwandan Patriotic Front.
Kabla ya sherehe hiyo, Rais aliongoza kikao cha mwisho cha Baraza la Mawaziri la serikali inayomaliza muda wake na baadaye aliwakaribisha kwa chakula cha mchana kuwashukuru kwa huduma yao.
Museveni alisema Baraza la Mawaziri lilikuwa na jukumu muhimu katika kusukuma Uganda kufikia hadhi ya nchi ya kipato cha kati.
Aliwashukuru wajumbe na Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri kwa kusimamia shughuli za serikali.
Uchaguzi mkuu uliandaliwa mwezi Januari mwaka huu nchini Uganda ambapo Museveni aliibuka mshindi katika kinyang’anyiro cha Urais akiwapiku washindani kadhaa akiwemo Bobi Wine.
Wine amaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi Ssentamu wa chama cha NUP na ambaye alikimbilia Marekani, alilalamika kwamba uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki.