Mwanamuziki wa Uganda Kalifah AgaNaga amepuuza madai kwamba tamasha yake ya hivi karibuni haikufanikiwa, akisisitiza kwamba ilifanikiwa kifedha.
Msanii huyo amesema alipata shilingi milioni 100 pesa za Uganda kutoka kwa tamasha hiyo akiongeza kwamba wanamitandao waliharakisha kuihukumu kwa kutumia picha zilizopigwa hata kabla yake kujapanda jukwaani.
AgaNaga alisema mauzo ya meza za VIP pekee yalichangia kiasi kikubwa cha fedha, kwani ziliuzwa kwa bei ya shilingi milioni 1,3 na 5.
Kulingana naye, mauzo ya meza 10 za milioni 3, tano za milioni 1 na nne za milioni 5 kulimwingizia mapato makubwa hata kabla ya kuhesabu mauzo ya tiketi za kawaida.
Kalifah aliongeza kuwa tiketi ziliuzwa kwa shilingi elfu 10, 20 na 30, akidai kuwa takribani watu 2,000 walihudhuria tamasha hiyo.
Mwimbaji huyo pia alidai kuwa taarifa hasi kuhusu tamasha yake zilichochewa na wivu uliotokana na kurejea kwa umaarufu wa wimbo wake wa Nassanga.
Aidha, alisema baadhi ya waandaaji wa matamasha hawakufurahishwa na uamuzi wake wa kuandaa tamasha hiyo mwenyewe badala ya kushirikiana nao.
AgaNaga alisema mafanikio ya tamasha yake aliyoliandaa mwenyewe yanaonyesha kuwa wasanii wenye nyimbo zinazovuma wanaweza kuandaa tamasha zao binafsi na kujipatia mapato moja kwa moja, akieleza kuwa huu ni mfumo wa biashara unaowapa wanamuziki udhibiti mkubwa zaidi wa taaluma zao.