Wakili wa Mahakama Kuu Alphonce Osewe alifikishwa mahakamani kuhusiana na sakata ya dhahabu ambapo yeye na mshirika wake wanadaiwa kujipatia mamilioni ya fedha.
Osewe alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu katika mahakama ya Milimani akikabiliwa na mashtaka ya kujipatia kitita cha shilingi milioni 69.02 kutoka kwa mlalamikaji kwa njia ya ulaghai.
Inadaiwa kwamba wakili huyo na mshirika wake walisingizia kuwa wanaweza wakamuuzia mlalamikaji dhahabu na hivyo kutia mfukoni fedha hizo bila kutimiza ahadi yao.
Ameshtakiwa kwa kupata pesa kwa njia ya udanganyifu, kinyume cha Sehemu ya 313 ya Kanuni ya Adhabu.
Wakili huyo alikamatwa na makachero katika ofisi ya kikanda ya DCI, eneo la Nairobi baada ya dhamana aliyopewa kufutwa alipokosa kufika mahakamani Oktoba 23, 2025.
Amekuwa akiwindwa tangu wakati huo.
Osewe amekanusha mashtaka huku mahakama ikiagiza aendelee kuzuiliwa hadi ombi lake la dhamana litakapoamuliwa.