Portable akamatwa na polisi

Polisi wa eneo la Kwara walithibitisha kukamatwa kwake kuhusiana na hatua yake ya kumtukana mwanamuziki mwenza kwa jina Osupa.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Nigeria Habeeb Okikiola maarufu kama Portable amekamatwa na polisi kufuatia malalamishi ya mwanamuziki wa mtindo wa Fuji Okunola Saheed maarufu kama Saheed Osupa.

Polisi wa eneo la Kwara walithibitisha kukamatwa kwake kuhusiana na hatua yake ya kumtukana Osupa.

Katika taarifa msemaji wa polisi wa Kwara Adetoun Ejire-Adeyemi, Osupa katika malalamishi yake, amemlaumu Portable kwa makosa kadhaa kama vile kumharibia sifa, kumtishia maisha, uchochezi, vitendo vya kuvuruga amani na matumizi ya lugha chafu.

Ejire-Adeyemi, alisema kwamba Portable alikamatwa katika eneo la Abeokuta, katika jimbo la Ogun jana Jumapili Aprili 13, 2025 na kuhamishiwa Ilorin, huku uchunguzi ukiendelea kuhusu madai dhidi yake.

Portable amesalia kizuizini hadi sasa akisubiri kufikishwa mahakamani.

Punde baada ya kutiwa mbaroni, Portable alitumia akaunti yake ya Instagram kusihi wafuasi wake waombe Osupa msamaha kwa niaba yake.

Picha za machapisho yake kwenye Insta Stories zimesambazwa mitandaoniambapo pia anadai kwamba tayari alikuwa amemwomba
mwimbaji huyo wa mtindo wa Fuji msamaha kupitia kwa watu kama Abu Abel.

Tuhuma dhidi ya Portable zinatokana na hatua yake ya kumtukana Osupa kufuatia hatua yake ya kuondoa wimbo wake kwenye majukwaa kadhaa ya mitandaoni kutokana na mwingilio wa hakimiliki.

Portable alimrejelea Osupa kama mtu mkubwa bure wakati akilalama hatua iliyowaghadhabisha mashabiki wa Osupa.

Website |  + posts
Share This Article