MC Nuvian ambaye ndiye mwandaaji wa tamasha iliyozua minong’ono mitandaoni kufuatia kile ambacho mwanamuziki Spice Diana alifanya, amezungumzia tukio hilo.
Nuvian anasema kwamba ameamua kujitokeza kuongea kuhusu yaliyotokea kwani amechagua kuyaangazia badala ya kujitetea.
Katika mahojiano, mwandalizi huyo wa tamasha alielezea kwamba kulikuwa na tatizo na tamasha hiyo toka mwanzo kwani hata mauzo ya tiketi hayakuafikia malengo yake ya awali.
Anasema hali hiyo ilimwacha bila pesa akashindwa kulipa watu kadhaa waliompa huduma na bidhaa kando na msanii Spice Diana.
Kulingana na Nuvian ni ukweli kwamba hakuwa amemlipa Spice Diana nusu ya pesa walizokubaliana alipofika katika eneo la tukio lakini anaamini hilo sio jambo ambalo lilimghadhabisha kiasi kile.
Nuvian anasema Spice alipofika eneo la tukio alikuwa na wakati mgumu kuingia kutokana na kutoelewana kati yake na usimamizi wa eneo hilo la burudani, na hapo ndipo hasira zake zilitokea.
Mwandaaji huyo wa tamasha anasema anataka kusuluhisha matatizo yalipo kati yake na Spice Diana kwani huenda watahitajiana katika siku za usoni.
Iwapo ulikosa habari hizo, Spice Diana wikendi iliyopita aliondoka sehemu fulani ya burudani katika wilaya ya Bukomansimbi na vifaa kama spika, vipaaza sauri na vipatakalishi kwa kukosa kulipwa nusu ya pesa zake.
Kabla ya hapo alikuwa amesimamisha tumbuizo katikati na kutoa onyo kwa mashabiki waliokuwepo na wasimamizi wa baa kwamba angekomesha tumbuizo kwakukosa kulipwa.
Baada ya kushawishiwa, alikubali kumaliza kutumbuiza lakini akaondoka na vifaa ambavyo alisema thamani yake ni sawa na pesa alizokuwa akidai.