Chama kimoja cha kisiasa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kimefikisha malalamiko yake kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na viongozi wa ukanda, kikidai kuwa raia wa Kongo wanakumbana na unyanyasaji na kutozwa fedha zisizo halali katika vituo vya mipakani.
Kupitia barua, Rais wa chama cha Debout Pour la Renaissance du Congo (DPRC), Roger Berthon Mibenge, anadai kuwa maafisa wa uhamiaji katika baadhi ya nchi wanachama wanatoza ada za visa kinyume cha utaratibu, hutumia vitisho, na wakati mwingine kuwazuilia wasafiri bila msingi wa kisheria.
Barua hiyo, iliyotumwa kwa Katibu Mkuu wa EAC na kunakiliwa kwa marais wa Uganda, Kenya, Tanzania, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Somalia, inaeleza kuwa mara nyingi wasafiri hulazimika kutoa fedha nyingi bila kupewa uthibitisho wowote wa malipo.
Aidha, waraka huo unaeleza kuwa wale wanaokataa kutoa fedha hizo hukabiliwa na vitisho, hukamatwa bila sababu za msingi, na huombwa fedha zaidi ili waweze kuachiwa huru.