Jamaa akamatwa kwa ulaghai unaohusu ardhi

Mohamed anadaiwa kumlaghai mwanamke huyo shilingi milioni 12 kwa kisingizio cha kumuuzia kipande cha ardhi mjini Garissa.

Marion Bosire
1 Min Read

Waafisa wa upelelezi wa kituo cha polisi cha Kilimani walimkamata mshukiwa mmoja kwa jina Abdi Yusuf Mohamed, wa umri wa miaka 44 anayelaumiwa kwa kumlaghai mwanamke fulani.

Mohamed anadaiwa kumlaghai mwanamke huyo shilingi milioni 12 kwa kisingizio cha kumuuzia kipande cha ardhi mjini Garissa.

Uchunguzi ulibaini kwamba Yusuf alipokea pesa hizo katika mafungu kupitia akaunti yake ya benki kati ya Juni 29 na Novemba 21, 2023.

Taarifa za kituo cha usajili wa ardhi mjini Garissa zilifichua ulaghai huo kwani zinaonyesha kwamba kipande husika cha ardhi kimesajiliwa kwa jina la mtu mwingine.

Mmiliki halisi wa ardhi hiyo amekuwa akishikilia umiliki wake tangu alipogawiwa na serikali.

Stakabadhi alizotoa Yusuf kuthibitisha umiliki wa ardhi hiyo zilibainika kuwa gushi na kufuatia hilo, maafisa walimsaka hadi maficho yake mtaani Eastleigh.

Alikamatwa jana Jumapili Aprili 13, 2025 na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Kilimani ambako angesalia hadi wakati wa kufikishwa mahakamani.

Idara ya upelelezi wa jinao inaonya wakenya wawe macho wanapotekeleza miamala inayohusu ardhi kupitia kwa kuthibitisha umiliki wa ardhi husika na uhalisia wa stakabadhi za umiliki.

Website |  + posts
Share This Article