Maelfu ya wajumbe kutoka mataifa manane ya Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), wanashiriki kongamano la kimataifa la Kiswahili linaloendelea katika uwanja wa Uhuru wa Kololo, viungani mwa jijini kuu la Kampala, Uganda.
Kongamano hilo ambalo limeanza leo na litakamilika tarehe 16 mwezi huu, linaandaliwa nchini Uganda kwa mara ya kwanza.
Shirika la Afrika Mashariki Fest, ndio waandalizi wa kongamano hilo linalowaleta pamoja wadau mbalimbali wakiwemo wahadhiri wa vyuo vikuu,wahandishi wa vitabu vya Kiswahili,Wanahabari na viongozi kutoka matabaka mbalimbali.
Uganda ilitwikwa jukumu la kuwa mwandalizi wa kongamano hilo mwaka uliopita wakati wa kongamano la kimataifa la Kiswahili mjini Havana, Cuba.
Lengo kuu la kongamano hilo ni kukuza na kueneza uzungumzaji wa Kiswahili Afrika Mashariki.
Mkereketwa wa Kiswahili kutoka Kenya Professa PLO Lumumba,mwandishi mashuhuri wa vitabu vya Kiswahili Mwalimu Wallah Bin Wallah ,washiriki kutoka Kenya na Wanahabari wakiongozwa na ujumbe wa kutoka shirika la utangazaji nchini KBC ni mingoni mwa wanaohudhuria kongamano.
Kaulimbiu ya kongamano la mwaka huu ni ’embracing Kiswahili a political and economic imperative for Africa’s Reinasance.'(Kukienzi Kiswahili wajibu wa kisiasa na kiuchumi kwa mvuvumko wa Afrika.)
Kongamano hilo linaandaliwa wakati makuzi ya Kiswahili yanakumbwa na vizingiti kadhaa vikiwemo lugha za asili,Sheng na kukosa kuwajibika kutoka kwa viongozi wa jumuia ya EAC kama lugha ya utangamano.
Wajumbe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,Tanzania,Ethiopia,Kenya pamoja na wenyeji Uganda wanahudhuria kongamano hilo.