Mke wa Jux Priscilla na rafiki yake Eni ambaye huwa wanaigiza naye wanaonekana kugeukia soko la Tanzania ili kupata watazamaji wa kazi zao.
Haya yalibainika kufuatia tangazo alilochapisha mitandaoni Eni la kuhimiza raia wa Tanzania watazame filamu yao iitwayo “All of Us” kwenye mtandao wa YouTube.
“Habari Familia yetu ya waswahili, Filamu yetu ya ‘ALL of US’ iliyotafsiriwa kwa maandishi ya Kiswahili inatoka ijumaa hii ya tarehe 20 mwezi huu, ikiwa katika ubora wa hali ya juu , yani pambeeeee.” alisema Eni katika chapisho hilo.
Aliendelea kwa kupigia debe kazi hiyo ya sanaa akisema, “Filamu hii ni nzuri sana na itapatikana kwenye youtube channel ya The Geng NG au Gusa link kwenye bio yangu ambayo itakupeleka moja kwa moja youtube kuitazama.”
Eni ana imani kwamba watakaoitazama wataipenda na kuifurahia huku akikiri mapenzi yake kwao.
Priscilla Ojo alifunga ndoa na mwanamuziki wa Tanzania Juma Jux hivi maajuzi na rafiki yake Eni alisafiri hadi Tanzania kuwa naye wakati wa hafla mbali mbali za ndoa.
Akiwa nchini Tanzania, Eni alitagusana na wabunifu mbali mbali ambapo alijaribu kujifunza Kiswahili kiasi cha kurekodi wimbo wa taifa hilo ambao aliimba kwa weledi.