Msongamano mkubwa wa magari umeshuhudiwa kwenye barabara kuu ya kutoka Nairobi kuelekea Thika baada ya gari la usafiri wa umma lililokuwa likisafirisha wanafunzi kuanguka.
Gari hilo lenye uwezo wa kubeba abiria 14, lililokuwa likielekea eneo la TRM, lilianguka karibu na Garden City.
Inaripotiwa kwamba dereva wa gari hilo alikuwa akiliendesha kwa kasi ya juu, akashindwa kulidhibithi na likaanguka huku shughuli za uokoaji zikianzishwa mara moja.
Video na picha zilizosambazwa mitandaoni zilionyesha wanafunzi waliokuwemo wakiwa wameketi kando ya barabara na waliojeruhiwa walipelekwa hospitalini kwa matibabu.
Msongamano huo mkubwa ulianzia eneo la Githurai 45 hadi Garden City na uliathiri pande zote mbili za barabara.
Gari husika lilikuwa la rangi ya waridi huku magari ya kusafirisha wanafunzi yakitakiwa kuwa ya rangi ya njano kulingana na maelekezo ya halmashauri ya uchukuzi na usalama barabarani NTSA.