Abi Chams azungumza baada ya kukosa tuzo ya BET

Msanii huyo wa umri mdogo amesema kwamba huu ndio mwanzo tu na ana ari ya kufanya vyema katika tasnia ya muziki.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Tanzania Abigail Chams maarufu kama Abi Chams amezungumza baada ya kukosa kushinda tuzo ya BET kinyume na matarajio yake na ya raia wa Tanzania.

Msanii huyo wa umri wa miaka 22 alikuwa ameteuliwa kuwania tuzo ya BET katika kitengo cha mwanamuziki mpya bora kimataifa yaani Best International Act.

Binti huyo alisafiri hadi Los Angeles, California nchini Marekani kwa hafla ya kutoa tuzo hizo iliyoandaliwa Jumatatu Juni 9, 2025 katika ukumbi wa Peacock.

Wakati kitengo chake kilifikiwa, alishangaa kusikia mwanamuziki wa Brazil kwa jina Ajulia Costa akiitwa jukwaani kama mshindi.

Awali wakati akimpigia debe mitandaoni, Katibu mkuu wa wizara ya habari utamaduni,sanaa na michezo nchini Tanzania Gerson Msigwa ambaye pia ni msemaji mkuu wa serikali alielezea kwamba kura za tuzo hizo ni ‘likes’ za chapisho la Chams kwenye Instagram.

Kulingana na wadadisi, chapisho la BET la Abi kwenye akauni yao rasmi ya Instagram lilikuwa na likes nyingi ikilinganishwa na zile za chapisho la Costa.

Leo kwenye akaunti yake ya Instagram Abi amesema kwamba tuzo za BET zimekuwa ukurasa muhimu sana maishani mwake akiongeza kwamba ameguswa sana na uungwaji mkono aliopata kutoka kwa Watanzania na hata watu wa nchi nyingine.

“Ninasonga mbele na furaha rohoni na moto katika moyo wangu – huu ndio mwanzo tu” aliendelea kusema msanii huyo ambaye aliandikisha historia ya kuwa msanii wa kwanza wa kike Afrika mashariki kuwahi kuteuliwa kuwania tuzo hizo.

Website |  + posts
Share This Article