Msanii wa muziki nchini Kenya Willy Paul amelaumu kampuni ya kusambaza umeme nchini KPLC kufuatia kile alichokitaja kuwa kuchomeka kwa mashine zake za studio ya muziki.
Kupitia Insta Stories msanii huyo alisema kwamba atataka malipo kutoka kwa kampuni hiyo kwani kila kitu kwa studio yake kimechomeka.
“KPLC ni lazima mnilipe!! Mashine zangu zote za studio hazipo tena!! Mmenichomea kila kitu kwa studio.” aliandika msanii huyo akiongeza kwamba sio yeye pekee aliathirika.
Kulingana naye, wakazi wote wa mtaa husika wameathirika akisema wamepoteza mali za thamani kubwa. “Sio mimi tu, mtaa mzima umepoteza mali zao za thamani!!!” aliandika.
Alimalizia ujumbe wake kwa maneno aliyoanzia yale ya kudai malipo kutoka kwa KPLC.
Willy Paul hakutoa maelezo ya kina lakini inaonekana kwamba hitilafu ya umeme ilikumba eneo ambapo studio yake ipo na kusababisha vifaa vya stima kuungua.