Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi nchini Uganda (UPDF) Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ametoa wito wa kubadilishwa kwa ufadhili wa kikosi cha Afrika Mashariki (EASF) na kuweka huru operesheni zake kwa mustakabali bora wa kanda hii.
Akizungumza leo Alhamisi kwenye mkutano wa 36 wa kawaida wa Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi Afrika Mashariki, Jenerali huo alisema ufadhili wa kikosi cha dharura cha Afrika Mashariki (EASF) kinapaswa kufadhiliwa na nchi wanachama na wala sio wafadhili kutoka nje.
Kwenye hotuba yake, Kaneirugaba alithibitisha kuwa Uganda itafadhili kikamilifu kikosi hicho, ili kushughulikia pengo la ufadhili lililopo.
“Ningependa kumfahamisha mkurugenzi kwamba, tutatekeleza jukumu letu kikamilifu kuhusiana na ufadhili,” alisema Jenerali huyo wa Uganda.
Mkuu huyo wa UPDF, alidokeza kuwa mkutano huo unaandaliwa wakati ambapo kanda hii inakabiliwa changamoto kadhaa.
Aidha, alimuomboleza Waziri wa Ulinzi wa Djibouti Hassan Omar Mohamed Bourhan, aliyefariki tarehe 16 Julai, huku akituma rambirambi kwa serikali, raia wa nchi hiyo na familia ya waziri huyo.