Wafugaji wa Trans Nzoia wanasababu ya kutabasamu, baada ya Idara ya Ustawi wa Mifugo kuwapa vifaranga 4,000 wa kienyeji walioimarishwa, kama hatua ya kupiga jeki ufugaji wa kuku na kuboresha maisha ya wakazi.
Vifaranga hao walikabidhiwa wakulima kwenye sherehe iliyoongozwa na maafisa wa Idara ya Ustawi wa Mfugo, Mwakilishi Mwanamke wa kaunti ya Trans Nzoia Lillian Siyoi, makundi ya wakulima na wadau wengine.
Hatua hiyo inalenga kuwezesha wakulima kupata kuku wa ufugaji wenye ubora wa hali ya juu, pamoja na kupanua biashara ya ufugaji kuku katika eneo hilo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, mwakilishi kutoka Idara ya Ustawi wa Mifugo aliwahimiza wakulima kutekeleza ufugaji wa kuku kama biashara na kuzingatia lishe mwafaka, usimamizi bora, kudhibti magonjwa ili kuwa na kuku wanaofikia kiwango cha soko.
Mpango huo ni sehemu ya mpango mpana wa kuimarisha sekta ya ufugaji, kuboresha utoshelevu wa chakula na kutoa fursa kwa wananchi kuwa na mapato kupitia biashara ya mifugo.